Friday, August 25 2017 at 14:56 (Gazeti Taifa Leo /KENYA)
Kwa Mukhtasari
MAGAVANA wameendelea kuwafuta kazi mawaziri na wafanyakazi wa kaunti zao. Gavana wa Meru Kiraitu Murungi alibandua bodi kadha Alhamisi jioni katika kile alichosema ni hatua ya kufichua makundi ya ufisadi ambayo yameteka kaunti hiyo.
Alichukua hatua hiyo siku moja baada ya Bw Murungi kuwasimamisha kazi mawaziri wake ili kutoa fursa ya kufanyika kwa ukaguzi wa fedha na wafanyakazi wa kaunti.
Hata hivyo, Bw Murungi aliwahakikishia wafanyakazi hao kwamba lengo la zoezi hilo si kuwaandama kwa sababu linatekelezwa kwa mujibu wa sheria.“Tuliahidi kuendelea na zoezi hili la kusafisha. Ndiposa tumebandua bodi na kubatilisha uteuzi wa wanachama wote wa bodi za mashirika mbalimbali ya kaunti,” akasema Bw Murungi.
Mashirika yaliyoathiriwa ni pamoja na lile la uwekezaji na ustawi, fedha, mapato na kudhibiti vileo.
Gavana pia alibandua kamati za usimamizi za hospitali, vituo vya afya na zahanati akisema hatua hiyo inaambatana na ahadi yake ya kufanyia mageuzi huduma za matibabu. Aliagiza maafisa wasimamizi wa vituo hivyo kuchukua usukani.
Bw Murungi alisema zoezi la ukaguzi litasaidia kuwang’oa wafanyakazi hewa.
“Tunajua kuna wafanyakazi hewa katika kaunti hii. Serikali iliyopita imekuwa ikilipa Sh15 milioni kwa vibarua kila mwezi, jambo ambalo linaibua shaka. Kuna vibarua 5,000 ilhali serikali ikon a wafanyakazi wa kutosha,” alieleza na kuongeza kuwa wafanyakazi ambao watakaopita ukaguzi watarejeshwa kazini.
Gavana wa Kisumu Prof Anyang’ Nyong’o aliwasimamisha kazi maafisa wakuu 14 na kuwaagiza wakurugenzi kuchukua usukani hadi wakuu wengine watakapoajiriwa.
Prof Nyong’o pia aliwafuta kazi mawaziri tisa wa kaunti.
Katika kaunti ya Nandi, Gavana Stephen Sang alibandua bodi ya usimamizi wa afya na kamati ya hospitali ya rufaa na zile za kaunti ndogo. Maafisa zaidi ya 40 waliathirika.
Vile vile alimsimamisha kazi waziri wa afya na maafisa wengine wakuu katika idara ya afya ili kutoa fursa ya uchunguzi wa kile alichodai ni kutoweka kwa fedha za idara hiyo.
Katika taarifa, Bw Sang alisema kuwa aliagiza idara ya ndani ya ukaguzi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mapato ambayo idara ya afya imekusanya katika miaka minne iliyopita.
Gavana wa Pokot Magharibi Prof. John Lonyangapuo amewapa likizo ya lazima wafanyikazi wakuu wa kaunti ili kutoa fursa ya uchunguzi kufanyika .
Katika kikao na wanahabari mjini Kapenguria, Prof Lonyangapuo alisema kuwa ameagiza mara moja ukaguzi wa idara za fedha na uajiri.
“Wafanyakazi wa ziada wamepunguzwa isipokuwa katika idara za afya na ukusanyaji ushuru. Lengo ni kuondoa wafanyakazi ghushi; baadhi waliajiriwa miezi michache kabla kampeni za uchaguzi kuanza,” alisema na kuongeza kuwa ukaguzi huo pia utahusu wanakandarasi.
Gavana wa Marsabit Mohamud Ali alisitisha shughuli katika wizara nane na kuagiza magari yote ya kaunti yapelekwe katika makao makuu ya kaunti.
“Nimesitisha shughuli katika wizara zote za kaunti isipokuwa zile za afya na maji,” alisema Bw Ali katika taarifa.
Gavana pia aliunda jopo kazi la wanachama tisa kuchunguza operesheni za Bodi ya Kuajiri Watumishi wa Umma (CPSB) katika miaka mitano iliyopita.
CHANZO:
Comments
Post a Comment