MKUU wa Mkoa wa Arusha,Tanzania, Mrisho Gambo amekiuka maagizo yaliyotolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu ya kutoa Sh milioni 20 kwa ajili ya kutunisha mfuko maalumu wa elimu ulioAnzishwa na Taasisi ya Stemm.
Kwa mujibu wa hotuba ya Makamu wa Rais iliyosomwa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mughwira wakati wa mapokezi ya watoto walionusurika kwenye ajali ya basi ya Shule ya Lucky Vincent, Doreen Mshana, Sadia Ismail na Wilson Tarimo waliorejea kutoka Marekani, serikali ilimwagiza Gambo kutoa kiasi hicho cha fedha ili kuunga mkono juhudi za taasisi hiyo iliyoahidi kusomesha watoto hao.
Hata hivyo, badala ya kuzielekeza katika taasisi hiyo, Gambo amezigawa fedha hizo kwa wazazi wa watoto hao walionusurika katika ajali hiyo bila masharti yoyote huku akiikana hotuba ya Mughwira kuwa hana fedha za ziada.
“Uongozi wa mkoa uliamua kuzigawa fedha hizo kiasi cha Sh milioni 23.2 ambapo familia za watoto watatu walionusurika ambao ni kila moja ilipata mgawo wa Sh milioni 7.7.
“Mkoa wa Arusha hauna hizo Sh milioni 20 mnachosema bali fedha zote zilizobaki ndiyo hizi ambazo tumewakabidhi wazazi wa watoto wetu hawa ambao Mwenyezi Mungu aliwanusuru kutokana na ajali iliyotokea bila masharti yoyote,” amesema Gambo.
Pamoja na mambo mengine, Gambo amesema fedha za michango ya rambirambi zilichangwa na wadau ikiwamo Serikali na watu binafsi ambapo amewalaumu baadhi ya wanasiasa akidai kuwa walipotosha kwa makusudi tukio la ajali hiyo kwa maslahi yao ya kisiasa.
CHANZO:
http://mtanzania.co.tz/gambo-agomea-agizo-la-makamu-wa-rais/
Comments
Post a Comment