IMEANDIKWA NA MALISA GJ :
Tundu Lissu ameeleza kuwa ni kweli ndege aina ya 'Bombadier Dash Q400' mali ya shirika la ndege la ATCL imeshikiliwa huko nchini Canada na kampuni moja ya Ujenzi ijulikanayo kama Stirling Civil Engineering Ltd kutokana na kuidai serikali ya tanzania kiasi cha USD 38M (Takribani TZS 87BL). Kampuni hiyo imetishia kuipiga "mnada" ndege hiyo kufidia deni lao, ikiwa serikali ya Tanzania haitawalipa.
KWANINI NDEGE YETU IMEKAMATWA?
Mwaka 2009 kampuni Stirling Civil Engineering Ltd, ilikupewa kandarasi ya kutengeneza Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo. Kabla ya kukamilisha kandarasi hiyo, aliyekuwa Waziri wa ujenzi wakati huo alivunja mikataba bila kuzingatia sheria, na kuinyang'anya kampuni hiyo kandarasi hiyo na kuagiza kampuni hiyo kutimuliwa nchini.
Kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd, ilifungua kesi katika mahakama ya kimataifa ya usuluhishi mjini Paris. Tarehe 10 Desemba, 2009 mahakama hiyo iliipa ushindi kampuni hiyo na kuagiza serikali ya Tanzania kuilipa takriban dola za Marekani milioni 25 (Takribani TZS 40BL kwa wakati huo).
Serikali ya Tanzania ilikata rufaa, lakini ikaangukia pua kwenye hukumu ya tarehe 10 Juni, 2010 ambapo mahakama hiyo iliagiza Tanzania ilipe fedha hiyo pamoja na riba ya 8% kila mwaka hadi malipo kamili yatakapofanyika. Tuzo hiyo imesajiliwa na kutambuliwa kama deni halali la Serikali ya Tanzania kwa Stirling Civil Engineering Ltd.
Lakini serikali ilikataa kulipa deni hilo, licha ya jitihada mbalimbali zilizofanywa na kampuni hiyo. Kutokana na ucheleweshaji wa malipo, deni hilo limeongezeka hadi dola za Marekani 38.7M kufikia tarehe 30 Juni, 2017.
Hapo ndipo Stirling Civil Engineering Ltd. ilipoamua kuomba amri ya Mahakama Kuu ya Montreal ya kukamata mali zote za serikali ya Tanzania zilizopo nchini Canada zikijumuisha ndege ya Bombardier Q400. Mahakama ilitoa kibali na ndege hiyo kukamatwa.
SERIKALI IMECHUKUA HATUA GANI?
Kwa mujibu wa Mhe.Tundu Lissu serikali iliomba mazungumzo na kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd ili kutatua tatizo hilo. Katika mazungumzo hayo ambapo serikali ya Tanzania iliwakilishwa na Waziri wa mambo ya nje Balozi Augustine Mahiga, aliomba kampuni hiyo kuepuka suala hilo kujulikana hadharani.
Kwa upande wake, kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd. imekubali kuiachia ndege ya Bombardier Q400 kwa malipo ya mwanzo ya dola za Marekani milioni 12.5 (Takribani TZS 30B) na baadae itatuma ujumbe wake Tanzania kwa ajili ya kuja kufanya makubaliano ya mwisho juu ya kulipa deni hilo. Endapo malipo hayo yatafanywa na Serikali, Stirling Civil Engineering Ltd, itasitisha mpango wake wa kuipiga mnada ndege yetu ya Bombardier Q400. Ikiwa serikali itashindwa kutimiza makubaliano hayo basi ndege hiyo itapigwa mnada.
Wakati huohuo kampuni ya uchimbaji madini ya ACACIA Mining imetoa notisi ya kuishitaki Serikali ili kudai fidia ya Dola za Marekani bilioni 2 (Takribani TZS Trilioni 5) kwa kukamata mchanga wake wa dhahabu, kinyume na sheria na mkataba wa uchimbaji madini waliosani na serikali.
Kampuni hiyo imetoa tishio hilo wakati mazungumzo yakiendelea kati yake na serikali juu ya hatma ya mchanga huo wa dhahabu maarufu kama makinikia. Ikiwa Accacia watafanyia kazi notisi hiyo, Tanzania itaburuzwa tena kwenye mahakama ya usuluhishi ya kimataifa, na kutakiwa kulipa Trilioni 5 kwa Accacia.
Nini maoni yako?
CHANZO:
https://m.facebook.com/story.php?story_fbid=1478370308921323&id=100002451047207
Comments
Post a Comment