MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Simba ya jijini Dar es Salaam kutoka Burundi, Laudit Mavugo, anatakiwa na klabu moja ya Ufaransa, Imeelezwa.
Mbali na klabu hiyo ya Ufaransa, pia mshambuliaji huyo wa Timu ya Taifa ya Burundi pia anatakiwa na timu nyingine inayoshiriki Ligi Kuu Serbia.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kutoka kwenye kambi ya Simba iliyoko Afrika Kusini jana, Mavugo alisema kuwa wakati wa kipindi cha likizo Juni mwaka huu alisafiri kwenda Serbia kwa ajili ya kufanya majaribio na alifaulu.
Mavugo alisema kikwazo cha klabu hiyo kuanza mchakato wa kumsajili ni kutokana na mkataba ambao bado anao na Simba na akiwa Afrika Kusini amepata taarifa kuwa klabu nyingine ya Daraja la Pili Ufaransa inamhitaji na imeshawasilisha barua kwa uongozi wa klabu yake.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa mabingwa wa Burundi, Vital'O ya jijini Bujumbura, alisema bado anaamini ana nafasi ya kwenda kucheza soka Ulaya na nafasi yake ya kusajiliwa na Simba imemuongezea uzoefu na kukuza kipaji chake.
"Meneja wangu bado anaendelea kunitafutia klabu za nje ya nchi, ndoto zangu bado hazijatimia, ila nilirejea Tanzania kwa sababu kuna watu wanaofahamu umuhimu wangu, sikuwa na wakati mzuri katika miezi ya kwanza niliposajiliwa, ila nilipambana kwa sababu nilijua ni changamoto za kawaida katika maisha yetu wachezaji," alisema mshambuliaji huyo.
Kiongozi mmoja wa juu wa Simba aliliambia gazeti hili kuwa ni kweli wakala wa mshambuliaji huyo ameanza mawasiliano na klabu hiyo, lakini wamemtaka aandike barua rasmi kwa ajili ya kuanza taratibu za kushughulikia ruhusa yake.
Aliongeza kuwa kwa sasa ni mapema kusema lolote kuhusiana na ofa ambazo mshambuliaji huyo amepata.
"Ni kweli wakala wake amewasiliana na sisi, lakini kulikuwa na changamoto ya lugha, ametuandikia kwa kifaransa, tumemtaka aandike barua rasmi ambayo tutaifanyia kazi," aliongeza kiongozi huyo.
Hata hivyo, taarifa za ndani za klabu hiyo zinasema kuwa Mavugo ambaye mkataba wake umebakiza mwaka mmoja ana nafasi ndogo ya kuruhusiwa kwenda kufanya majaribio nje ya nchi kutokana na Simba kuhitaji mafanikio zaidi katika msimu ujao na mashindano ya Kombe la Shirikisho watakayoshiriki hapo mwakani.
CHANZO:
http://m.ippmedia.com/sw/michezo/mavugo-atakiwa-ufaransa-serbia
Comments
Post a Comment