|
Baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe kupinga maoni ya Mbunge wa Singida Mashariki, Raisi wa chama cha wanasheri wa Tanganyika na mwanasheria mkuu wa CHADEMA ya kutaka Jumuia ya kimataifa kuinyima misaada Tanzania kutokana na ukiukwaji wa haki za kibinadamu, Leo hii Mh.Zitto Kabwe ametolea ufafanuzi maoni yake kupitia kwenye ukurasa wake wa Facebook.
UJUMBE HUO UNASOMEKA HIVI:
Tupeane maarifa tu kidogo. Duniani kote Nchi inapokatiwa Misaada watawala hutumia fursa hiyo kujenga hoja za kizalendo kuwa hatuendelei kwa sababu tumekatiwa misaada. Zimbabwe ni mfano mzuri sana juu ya jambo hili. Burundi ndio hali inayoendelea hivi sasa.
Hapa Tanzania hali ya Uchumi ni mbaya sana, mbaya mno. Uzalishaji umeshuka, kote mashambani na viwandani. Uzalishaji kwenye kilimo umeshuka mpaka kufikia 0.6% kwa mwaka mpaka 2.5% kwa mwaka, Uzalishaji Viwandani umeshuka kwa karibu 50%. Mapato ya wananchi yameshuka sana. Hivyo kila mwananchi anajua kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kabisa kuendesha uchumi wa nchi.
Kutaka misaada ikatwe ni kuwapa watawala hawa kisingizio cha kushindwa kuendesha Uchumi kwa sababu ya sera mbaya. Misaada ikikatwa Watawala watasema "hatuendelei Kwa sababu tumekatiwa misaada, kwa sababu ya vita ya kiuchumi (msamiati wa kimkakati ambao washaanza kuutumia)", wakati hali halisi ni kuwa wameshindwa kuendesha Uchumi.
Kwanini muwape watawala visingizio wakati uchumi huu utaanguka tu kwa uendeshaji mbaya? Kiongozi yeyote mwenye akili timamu na mwenye kutazama mambo kimkakati hawezi kutaka misaada ikatwe bali atawaeleza wananchi kuwa uchumi unaporomoka kwa sababu ya sera mbaya na kwa sababu watu hawana Uhuru na demokrasia, maana uhuru wa demokrasia huleta mezani mawazo, sera na mbinu mbadala za kuendesha uchumi, tofauti na hali ilivyo sasa.
Hatupaswi kamwe kuingiza wageni kwenye jambo hili. Tunaliweza wenyewe.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama - ACT Wazalendo
Kigoma
Julai 20, 2017
VYANZO:
https://m.facebook.com/story.php?story_fbid=1751968155101229&substory_index=0&id=1553424368288943
Comments
Post a Comment