PENGINE ilikuwa si rahisi kufikiri hapo kabla kuwa ipo siku mwenyekiti wa chama tawala anaweza kusema ukweli wenye kugusa maslahi ya mbunge wa chama chake kunako mkutano wa hadhara.
Hata hivyo, jambo hilo si la kushangaza tena katika serikali ya awamu ya tano iliyopania kusimamia misingi ya ukweli kwa maslahi mapana ya taifa.
Hali hiyo ilijidhihirisha jana mjini Morogoro wakati Rais John Magufuli alipomlipua mbele ya mkutano wa hadhara Mbunge wa Morogoro Mjini (CCM), Aziz Abood, kwa kumtaja kuwa miongoni mwa watu waliotwaa viwanda mkoani humo na baadhi yake kuvigeuza kuwa machungio ya mbuzi badala ya kuviendeleza kama ilivyotarajiwa.
Jana, akizungumzia agizo hilo la Rais Magufuli, Abood ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya mabasi ya Abood iliyopo mkoani humo, alisema anatekeleza agizo la Rais na tayari kiwanda chake cha Moproco kimefunga mashine mpya kwa ajili ya uzalishaji.
Akizungumza katika mkutano wake huo kwenye eneo la Msamvu mjini Morogoro jana, Rais Magufuli (JPM), ambaye pia mwenyekiti wa taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema Abood na watu wengine waliomilikishwa viwanda na serikali wanapaswa kuviendeleza au kuvirejesha serikalini ili wapewe wawekezaji wengine waviendeleze.
Rais Magufuli aliyasema hayo wakati akizungumza baada ya kusimama Msamvu kwa muda akitokea Dodoma kwenda jijini Dar es Salaam.
“Ninarudia wito wangu niliokwisha kuutoa huko nyuma, kwamba wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendesha wavirejeshe serikalini. Na leo nataja, akiwemo Mbunge wa hapa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)… narudia, akiwamo Mbunge wa hapa wa CCM ambaye alibinafsishiwa viwanda vingi.
“Alipewa viwanda vingi na sasa nasikia anafugia mbuzi… sasa kama ameshindwa kuviendesha avirudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:
“Nazungumza kwa uwazi kwa sababu msemakweli ni mpenzi wa Mungu.”
Rais Magufuli alisisitiza kuwa suala la kusimamia ukweli kwa manufaa ya taifa halichagui itikadi ya chama na ndiyo maana analisema hilo bila kificho.
“Uwe CCM, uwe CUF uwe Chadema, ukifanya ya ovyo mimi nakutandika tu, tena hadharani. Kwa hiyo mheshimiwa Mbunge wa hapa nampenda… na ni mbunge wa chama changu, lakini nataka viwanda alivyopewa vifanye kazi,” alisema Rais Magufuli na kuibua shangwe kubwa kutoka kwa mamia ya wananchi waliokuwa wakimsikiliza.
Kwenye mkutano huo, Rais Magufuli aliwapongeza pia wakulima wa mazao katika mkoa wa Morogoro kwa kuongeza uzalishaji.
Aidha, alimwagiza Kamanda wa Polisi wa Morogoro, SACP Ulrich Matei, kuhakikisha askari mgambo hawawasumbui wafanyabiashara wa Msamvu.
ABOOD AFUNGUKA
Akizungumza na Nipashe jana kuhusiana na maelekezo ya Rais juu ya viwanda alivyobinafsisha, Abood alisema anatekeleza na kiwanda anachomiliki cha Moproco kimeshaanza kufanya kazi.
Alisema mashine za kiwanda hicho zimeshafungwa na kwamba, kwa sasa kinachosubiriwa ni leseni tu.
“Rais Magufuli anahimiza, na sisi tunajitahidi kufuata kauli zake. Jitihada zinafanyika ili kila kitu kiende sawa na vijana wetu wapate ajira.
Morogoro kuna viwanda vingi ambavyo vitafunguliwa… siyo vya kwangu tu, Rais Magufuli anatumihimiza wote wenye viwanda,” alisema Abood.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2012 ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) , takribani viwanda na mashirika 17 ya umma nchini yaliyobinafsishwa mwaka 1993 yamefungwa baada ya kushindwa kuzalisha.
CHANZO:
http://m.ippmedia.com/sw/habari/jpm-alivyomlipua-abood-wa-mabasi
Comments
Post a Comment